Obama :Sudani kusini iko hatarini

Image caption Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir

Rais wa Marekani, Barack Obama ameonya kuwa Sudani kusini iko katika hatari ya kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, baada ya kutokea mapigano mjini Juba.

Amesema kuwa Wanajeshi 45 wamepelekwa nchini Sudani kusini siku ya jumatano kwa ajili ya kuwalinda Raia wa Marekani na mali zao.

Obama amesema kuwa hali ya sasa nchini Sudani kusini inatishia kulirudisha taifa hilo katika miaka ya nyuma, akitoa wito kukoma kwa vitendo vya uchochezi na mashambulizi miongoni mwa jamii hizo na kuzitaka jamii hizo mbili kufanya mazungumzo kuondoa tofauti zao.

Takriban watu 500 wanahofiwa kupoteza maisha tangu mwishoni mwa juma lililopita, wakati Rais wan chi hiyo Salva Kiir alipomtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwa kutekeleza jaribio la kupindua Serikali.

Image caption Riek Machar anatuhumiwa kujaribu kumpindua Kiir

Takriban watu 34,000 wameomba hifadhi ya ukimbizi katika maeneo ya ofisi za Umoja wa mataifa.

Walinda Amani wenye asili ya India waliuawa siku ya Alhamisi kambi ya Umoja wa Mataifa inayohifadhi wakimbizi iliposhambuliwa katika eneo la mpaka kati ya Sudani kusini na Ethiopia, jimboni Jonglei.

Akitoa taarifa kuhusu vifo hivyo katika mkutano wa UN jijini New York, Balozi wa India ndani ya UN Ashok Mukeriji amesema kuwa mashambulizi ya siku ya Alhamisi yaliyotekelezwa na vijana wa jamii ya Nuer katika kambi yao yaliwalenga wao .

Sudani ilipitia kipindi cha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 22,mapigano yaliyogharimu maisha ya Zaidi ya watu milioni moja kabla ya Sudani kusini kupata uhuru wake mwaka 2011.

Mgogoro wa sasa unahusisha jamii ya Nuer anakotoka Machar na Dinka anakotoka Kiir.

Image caption Maelfu ya Raia wamekimbia mapigano nchini humo

Rais Kiir ameshutumu vikosi vinavyomuunga mkono Machar kuwa vimekuwa vikifanya mashambulizi nchini humo.

Machar amekana shutma kuwa alikuwa na mipango ya kuipindua Serikali ya nchi hiyo.

Ingawa wito umekuwa ukitolewa kutaka utulivu miongoni mwa makundi hayo hasimu, bado mapigano yameendelea katika mji wa Bor jimbo la Jonglei kaskazini mwa Juba.

Msemaji wa Umoja wa Afrika Ateny Wek Ateny amesema kuwa mji wa Bor unadhibitiwa na vikosi vitiifu kwa Machar hata hivyo Vikosi vya Serikali vinafanya jitihada ya kuurejesha mji huo kwenye himaya yao.