Ulipizaji kisasi wazidi Sudan Kusini

Wageni wakisaidiwa kuondoka Sudan Kusini

Mratibu wa shughuli za Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, Toby Lanzer, ameiambia BBC kwamba malaki ya watu wanahofia maisha yao huku ghasia za kikabila zikiongezeka.

Mapigano yalizuka juma lilopita baina ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomuunga mkono makamo wa rais wa zamani, Riek Machar.

Bwana Lanzer alisema aliona watu wakiuliwa mabara-barani na wengine wakikimbilia kwenye eneo la majengo ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Bor ambako mapigano yanaendelea.

Alisema kuna hali ya hofu kubwa na mashambulio ya kulipiza kisasi yamezidi.

Jeshi la Sudan Kusini limethibitisha kuwa Bentiu, mji mkuu wa jimbo la Unity linalotoa mafuta, umetekwa na wanajeshi walioasi na watiifu kwa Riek Machar.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini unasema unawahamisha wafanya-kazi wote wasiokuwa muhimu.

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague, amelaani ghasia hizo na kusema kuwa zinakwenda kinyume na matumaini ambayo ndiyo yalikuwa msingi wakati taifa jipya lilipoundwa mwaka wa 2011.