Watu 1000 wakisiwa kuuwawa Sudan Kusini

Rais Desalegn wa Ethiopia, Kiir wa Sudan Kui na Kenyatta wa Kenya wakikutana mjini Juba

Mapigano makali yanaendelea Sudan Kusini, baina ya wanajeshi wa serikali ya Rais Salva Kiir, na wale watiifu kwa makamo wa rais wa zamani, Riak Machar.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa, Hilde Johnson, anasema watu zaidi ya elfu moja wameuwawa, ingawa idadi hasa haijulikani.

Viongozi wa Afrika wanajaribu kupatanisha na Rais Salva Kiir amekutana na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, na waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

Ripoti zinasema viongozi hao wamejadili juu ya uwezekano wa kusitisha mapigano, mazungumzo ya kutafuta amani, na maafa ya raia hivi sasa.

Haijulikani kama viongozi wa Ethiopia na Kenya watakutana na Bwana Riek Machar piya.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi anaeleza kuwa Sudan Kusini ni muhimu kibiashara kwa jirani zake.

Kenya imeiuzia nchi hiyo bidhaa za thamani ya dola 290 milioni mwaka huu.

Serikali ya Kenya inasema raia wake kama 1,000 bado wamenasa katika miji ya Sudan Kusini - wafanya-biashara, walimu, wafanyakazi katika usalama na wachuuzi.

Piya kuna wasiwasi kuwa mapigano yakizidi yataakhirisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ya Sudan Kusini hadi bandari ya Lamu, Kenya.