Viongozi wa A.Mashariki kukutana

Image caption Rais wa Sudani kusini Salva Kiir

Viongozi kutoka Afrika mashariki wanatarajia kukutana nchini Kenya kujadili kuhusu machafuko yanayokithiri nchini Sudani kusini, ambapo zaidi ya Watu 1,000 wanaaminika kupoteza maisha.Mazungumzo hayo yanakuja siku moja baada ya Rais wa Sudani kusini Salva Kiir kukutana na Mawaziri wakuu kutoka nchini Kenya na Ethiopia.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema kuwa kikosi cha kwanza cha kulinda amani kinatarajiwa kuwasili nchini Sudani kusini saa kadhaa zijazo.machafuko yalijitokeza siku 12 zilizopita kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Kiir na vile vinavyomuunga mkono aliyekuwa naibu wa Kiir, Riek Machar. Zaidi ya raia 50,000 wamekimbia makazi yao na kuomba hifadhi katika Ofisi za UN huko Sudani kusini.

Viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki kutoka jumuia ya Igad watakutana jijini Nairobi kwa ajili ya kujadili maswala yaliyogusiwa katika mazungumzo yaliyofanyika siku ya Alhamisi kati ya Rais Kiir na Viongozi hao jijini Juba.

Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Habari wa Sudani kusini Makuei Lueth ameliambia shirika la habari la AP kuwa mpaka sasa hakuna mawasiliano na Machar.

Sudani kusini imekuwa ikipigania kupata Serikali thabiti tangu kupata uhuru wao mwaka 2011, baada ya kujitenga.