Raia wa Chad wakimbia Afrika ya Kati

Image caption mwanajeshi wa Ufaransa wa kulinda amani Jumuhuri ya Afrika ya Kati

Maelfu ya raia wa Chad wanakimbia machafuko nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati na wamekuwa wakiondoka nchini humo siku ya Jumamosi na kujiunga na maelfu ya raia waliondoka wiki iliyopita.

Raia wa Chad waliokuwa wanaishi nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wamekuwa wakituhumiwa kwamba baadhi yao wamekuwa wakiwasaidia waasi wanaoipinga serikali yaani kundi la wapiganaji la Seleka.

Pia madai kama hayo yameelekezwa kwa askari wa Chad waliopo ndani ya kikosi cha Umoja wa Mataifa kilichopo nchi Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Nchi ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati ilikubwa na machafuko tangu mwezi marchi wakati waasi wa Seleka walipompindua Rais wa nchi hiyo Francois Bozize.

Uhasama ulizidi kupamba moto zaidi hasa pale waasi wa Seleka ambao wengi wao ni waislamu walipoanza kupambana na makundi ya wakristo.

Waislamu kutoka Afrika ya Kati ni miongoni mwa walioripotiwa kukimbia nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Afrika AU imetuma askari wapatao 4,000 nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wakati Ufaransa ambayo iliwahi kuitawala nchi hiyo nayo imepeleka wanajeshi wapatao 1,600.

Inasadikiwa mamia ya raia wa Chad wanaoishi nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wengi wao ni wale ambao familia zao ziliiishi nchini humo kwa vizazi kadhaa vilivyopita.

Wakristo wengi wanaishutumu serikali ya Chad ambayo wengi ya raia wake ni waislamu kwamba wamekuwa wakiwasaidia wapiganaji wa Seleka.

Siku ya Jumatano wanajeshi sita wa Chad waliopo kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani waliuawa kwa shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa Kikristo wanaojulikana Anti Balaka katika mji mkuu wa Bangui.

Raia wa Chad waliokuwa wanaondoka katika mji wa Bangui siku ya jumamosi walikuwa wakilindwa na majeshi ya Ufaransa dhidi ya wapiganaji.

Tayari raia wa Chad wapatao 2,743 wameondoaka nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati katika wiki za hivi karibuni taarifa hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji International Organisation for Migration (IOM).