Jeshi jeupe larudi nyuma Sudan Kusini

Waziri wa habari wa Sudan Kusini, MIchael Makuei

Serikali ya Sudan Kusini inasema wengi kati ya maelfu ya vijana ambao waliarifiwa kuwa wanaelekea mji muhimu wa Bor, sasa wameshawishiwa warudi nyumbani.

Waziri wa habari Michael Makuei ameiambia BBC kwamba wanasiasa wa kabila na Nuer katika eneo hilo, wameingilia kati kuwazuwia vijana hao kuelekea Bor - mji uliokombolewa na jeshi la serikali.

Hapo awali ofisi ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini ilisema helikopta yao iliyokwenda kupeleleza, kuangalia nyendo za kundi hilo la wanamgambo kama kilomita 50 kaskazini-mashariki ya Bor, iliwakuta lakini hawakujua idadi hasa.

Vijana hao wanaitwa "jeshi jeupe" kwa sababu ya jivu wanalojipaka kujikinga na wadudu.

Watu zaidi ya 1,000 wamekufa katika mapigano ya kikabila ya majuma mawili.

Wapatanishi wa Afrika Mashariki wamemuomba Rais Salva Kiir na makamo wake wa zamani, Riek Machar, wasitishe mapigano kati ya wafuasi wao ifikapo Jumaane.