Jeshi larejesha hali ya utulivu,Kinshasa

Image caption Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo limesema kuwa limefanikiwa kuzima shambulio lililolenga uwanja wa ndege na kituo cha taifa cha Radio na Televisheni linalodaiwa kutekelezwa na kundi lisilofahamika la kigaidi.

Waziri wa habari nchini humo, Lambert Mende, amesema kwa sasa hali imedhibitiwa na kuwaua watu 40 miongoni mwa waliokuwa wakiendesha mashambulio hayo.

Watu hao waliokuwa na silaha 16 kati yao wameuawa katika mapambano na polisi uwanja wa ndege,16 wengine katika eneo la jeshi na nane wao waliuawa katika ofisi za Radio ya Taifa.

Amesema kuwa kulikuwa na matukio mengine mawili ya mashambulio katika maeneo ya uwanja wa ndege na kambi ya jeshi.

Kwa mjibu wa Waziri Mende watu hao waliokuwa wakiendesha mashambulio hayo katika televisheni ya taifa na makao makuu ya radio ya taifa walikuwa na silaha zikiwemo bunduki,visu lakini walidhibitiwa kabla ya kusababisha madhara.

Mashambulio haya yametokea wakati Rais Joseph Kabila akiwa ziarani katika jimbo la Katanga nchini humo.

Ubalozi wa Marekani umetoa tahadhari kwa raia wake kutofanya safari za ndani ya mji wa Kinshasa hadi hali itakapodhibitiwa zaidi.