Tembo wazidi kuuawa Tanzania

Mauaji ya tembo yadaiwa kuongezeka nchini Tanzania tangu serikali ya nchi hiyo isitishe Opereshieni Tokomeza Ujangili kutokana na kuwepo madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Lazaro Nyarandu amesema idadi ya tembo 60 wameuawa katika kipindi cha miezi miwili tu ya mwezi Novemba na Desemba ikilinganishwa na tembo wawili tu waliouawa mwezi wa kumi mwaka huu

Hata hivyo idara za ulinzi zilikubaliana kuwaua majangili watakaobainika wakiwaua tembo hao kipindi ambacho msako huo ulikuwa ukiendelea mwezi Oktoba mwaka huu

Serikali ilisitisha operesheni hiyo kufuatia malalamiko kwamba watekelezaji wa msako huo walikuwa wakikiuka haki za binadamu, kwa mujibu wa kamati ya bunge iliyoundwa kufuatilia malalamiko hayo.

Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda alikaririwa akisema operesheni hiyo ilikuwa na nia njema lakini taarifa za kuwepo vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu ndicho ambacho hakikubaliki na serikali.

Matokeo ya uchunguzi wa kamati maalumu kuhusiana na kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu ndiyo uliosababisha Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kuwawajibisha kisiasa mawaziri wanne, akiwemo Shamsi Vuai Nahodha wa jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi Mambo ya Ndani, Waziri wa Utalii na Maliasili Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo Dr. Mathayo David Mathayo.

Baadhi ya nchi za bara la Asia zinazodaiwa kujihusisha zaidi na biashara ya pembe za ndovu hali inayoongeza kasi ya ujangili na mauaji ya tembo nchini Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.