Hali ya Schumacher yaimarika

Image caption Michael Schumacher apata ajali kwenye milima ya Alps, Ufaransa

Madaktari wa bingwa wa zamani wa mbio za magari ya langa langa, Michael Schumacher, wamesema hali yake imeimarika kiasi baada ya kufanyiwa upasuaji kupunguza shinikizo katika ubongo wake.

Kipimo kipya cha uchunguzi kilichochukuliwa usiku kucha kimeonyesha dalili kwamba hali yake ni "nzuri zaidi kuliko ilivyokuwa jana", lakini bado hajawa salama, wamesema madaktari hao.

Bingwa huyo mara saba wa mbio za magari ya langa langa ya Formula 1 alipata majeraha ya kichwa Jumapili wakati wa mchezo wa kuruka katika theluji kwenye milima ya Alps nchini Ufaransa.

Aliwekwa katika uangalizi mkubwa wa matibabu.

Kipimo cha kwanza kilichofanyika Jumatatu usiku kilionyesha, kuimarika kwa hali yake na kutoa fursa ya kufanyika upasuaji wa pili, wamesema madaktari.

Familia walichukua uamuzi mgumu wa kuwaruhusu madaktari kuendelea na upasuaji huo, na madaktari walifanya kazi hiyo ya upasuaji kwa saa mbili.

Habari za ajali aliyopata Schumacher wakati akicheza mchezo wa kuteleza katika theluji kwenye milima ya Alps nchini Ufaransa, zilitawala katika vyombo vya habari vya Ujerumani.

Schumacher alikuwa akiteleza kwenye theluji na mtoto wake wa kiume, wakati alipoanguka na kujipigiza kichwa katika mwamba.

Alikimbizwa katika hospitali ya karibu ya mji wa Moutiers. Baadaye alihamishiwa katika hospitali kubwa ya Grenoble.

Msemaji wa Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kiongozi huyo na serikali yake, kama ilivyo kwa mamilioni ya wananchi wa Ujerumani, wameshitushwa mno na taarifa za ajali ya Michael Schumacher.

"Tuna matumaini kwamba Michael Schumacher na familia yake wataweza kukabiliana na hali hii na kupona, amesema msemaji wa Chansela Angela Merkel.

Mchezaji mwenzake wa zamani katika timu ya magari la langa langa ya Ferrari, Felipe Massa, ambaye aliponea chupuchupu kupoteza maisha baada ya kupata ajali wakati wa mashindano ya Hungarian Grand Prix, ya mwaka 2009, ametuma ujumbe katika Instagram: "Nakuombea kaka yangu! Nina matumaini kwamba utapona haraka! Mungu akubariki, Michael."

Jumatatu, baadhi ya wapenzi na mashabiki wa Michael Schumacher walikusanyika nje ya hospitali ya Grenoble.

Nuravil Raimbekov, mwanafunzi kutoka Kyrgyzstan ambaye anasoma karibu na hospitali hiyo, amemwelezea Schumacher kama kivutio. "Nina wasiwasi, bila shaka... Lakini bado nina matumaini, na nitaomba kwa ajili yake," amesema mwanafunzi huyo.