Sudan Kusini wakubali mazungumzo

Image caption Wapiganaji wa Sudan Kusini

Pande mbili zinazopigana katika mgogoro wa Sudan Kusini zimekubali kukukatana nchini Ethiopia kwa ajili ya mazungumzo ya amani, lakini kiongozi wa waasi, Riek Machar, ameiambia BBC kuwa hatasitisha mapigano dhidi ya majeshi ya serikali.

Pia amesema majeshi yake yametwaa tena mji muhimu wa Bor kutoka majeshi ya serikali -- lakini madai haya hayajathibitishwa.

Waasi waliushambulia mji huo saa chache kabla ya kumalizika kwa muda uliwekwa na viongozi wa Afrika Mashariki, kwa kuzitaka pande zinazopingana nchini Sudan Kusini kukubaliana kumaliza uhasama kati yao -- au wakabiliwe na majeshi ya nje kwa kuingilia kati mgogoro huo.

Bwana Machar awali alikaririwa akisema asingeingia katika mazungumzo ya amani hadi hapo washirika wake wa kisiasa wanaoshikiliwa na serikali watakapoachiliwa huru.

Mapigano kati ya waasi na askari watiifu kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, yameenea nchini kote katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.