Milipuko miwili yatikisa Mugadishu

Magari mawili yamelipuka nje ya hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kuwaua watu 10.

Milipuko hiyo ilitokea katika hoteli ya Jazeera ambayo hutembelewa na wanasiasa pamoja na raia wa kigeni.

Duru zinasema kuwa milipuko ilifuatiwa na ufyatulianaji risasi kati ya maafisa wa usalama na washambuliaji.

Kundi la wanamgambo wa kiisilamu la al-Shabab, ambalo liliondoshwa Mogadishu mwaka 2011, limekiri kufanya shambulizi hilo.

Kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaeda bado linadhibiti sehemu kubwa ya Kusini mwa Somalia na maeneo mengine ya kati na limekuwa likiendelea kufanya mashambulizi ya kuvizia mjini Mogadishu.

Maafisa wanne wa usalama ni miongoni mwa watu waliofariki, akiwemo afisaa mwingine mmoja mkuu.

Afisaa wa polisi Mohamed Warsame aliambia shirika la habari la AFP kwamba bomu la pili lililipuka wakati maafisa wa usalama walipokuwa wanawasaidia waathiriwa wa shambulizi la kwanza

Hoteli ya Jazeera ambayo iko karibu na uwanja wa ndege, iliwahi kulengwa kwa shambulizi Disemba mwaka 2012, wakati Rais Hassan Sheikh Mohamud alipokuwa anaishi katika hoteli yenyewe. Watu saba walifariki wakati wa shambulizi hilo.

Wiki jana angalau watu 11 wakiwemo wanajeshi sita waliuawa katika shambulizi lengine la bomu mjini Mogadishu.

Al-Shabaab ni kundi lililoharamishwa na Marekani pamoja na Uingerzea na linaaminika kuwa na kati ya wapiganaji 7,000 na 9,000.

Licha ya kuwa limepoteza udhibiti wa miji kadhaa bado linaendesha harakati zake katika sehemu kubza za nchi hiyo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii