Waziri mkuu wa India kustaafu siasa

Image caption Waziri mkuu wa India Manhoman Singh

Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, amesema hatawania muhula wa tatu kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Waziri huyo mkuu amesema atamkabithi mamlaka ya nchi waziri mkuu mpya ikiwa chama chake cha Congress kitashinda uchaguzi huo utakaoandaliwa miezi michache ijayo.

Bwana Singh amesema chama cha Congress kitamtaja mgombea wake hivi karibuni na kusema naibu kiongozi wa chama hicho kwa sasa raul Gandhi ana tajiriba na uzoefu wa kazi kuweza kuteuliwa.

Serikali yake ambayo ni muungano wa vyama , imekuwa ikikosolewa mara kwa mara kwa tuhuma za ufisadi na kashfa nyinginezo.

Singh alisema kuwa litakuwa jambo baya sana ikiwa kiongozi wa upinzani Narendra Modi atachaguliwa kama waziri mkuu mpya.

Modi anaongoza chama cha upinzani Bharatiya Janata ambacho hivi karibuni kilishinda uchaguzi wa wabunge katika majimbo manne muhimu.

"Mtu aliyeendesha mauaji ya halaiki ya watu wasiokuwa na hatia, hapaswi kuchaguliwa kama waziri mkuu,'' alisema bwana Singh.

Modi ni gavana wa jimbo la Gujarat na ametuhumiwa kwa kukosa kuchukua hatua za kutosha kukomesha ghasia za kidini dhidi ya waisilamu ambazo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000. Hata hivyo Bwana Modi amekuwa akikanusha kuhusika na ghasia hizo.