Wahamiaji waokolewa pwani ya Ulaya

Image caption Wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini wakiwasili katika kisiwa cha Lampedusa cha Italia wakisindikizwa na walinzi wa pwani ya nchi hiyo.

Wahamiaji zaidi ya 300 wameokolewa kutoka pwani za bahari nchini Italia na Ugiriki katika matukio tofauti.

Jeshi la wanamaji la Italia limesema liliwaokoa watu 233, wengi wao wakitoka nchi za Afrika, ambao walikwama katika mashua zilizokuwa na msongamano mkubwa wa watu kusini mwa Sicilia.

Wakati huo huo walinzi wa pwani wa Ugiriki waliwaokoa wahamiaji 85 katika pwani ya kisiwa cha Astypalaia.

Kila mwaka maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika na Kiarabu wanaokimbia vita na umaskini, wanahatarisha maisha yao kwa kujaribu kwenda Ulaya wakitumia vyombo duni vya usafiri na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Ugiriki na Italia ni vituo vikubwa vinavyotumiwa na wahamiaji kujaribu kuingia barani Ulaya kwa kufanya safari za hatari za kuvuka bahari.

Mwezi Oktoba, 2013 zaidi ya watu 400 walikufa kwa kuzama baharini katika matukio mawili karibu na kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.

Wengi wao walikuwa wakitoka Eritrea na Somalia, lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, pia navyo vimesababisha kuongezeka kwa wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya.

Maafisa wa Italia wamesema Alhamisi kuwa wahamiaji waliokolewa kutoka katika mashua waliyokuwa wakisafiria yenye urefu wa mita kumi, ikiwa umbali wa kilomita 130 kutoka Lampedusa.

Image caption Ramani ya wahamiaji kuingia Ulaya

Taarifa ya maafisa hao imesema wahamiaji hao walikuwa na afya njema na walisafirishwa hadi Sicilia.

Wameripotiwa kuwa wametoka nchi za Eritrea, Nigeria, Somalia, Zambia, Mali na Pakistan.

Maafisa wa Ugiriki nao wanasema waliwaokoa wahamiaji karibu na Astypalaia baada ya kupata ishara ya hatari kutoka kwa nahodha wa mashua waliyokuwa wakisafiria kutokana na hali mbaya ya hewa baharini.

Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliokolewa.

Katika siku zilizopita, mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, yalizikosoa nchi za Italia na Ugiriki kwa sera zao za kuwarejesha wahamiaji hadi maeneo walikotokea.

Baada ya tukio la Lampedusa, serikali ya Italia ilianzisha operesheni ya kuzuia maafa zaidi kwa wahamiaji, kwa kuandaa meli za kivita na ndege ili kutumika kuwaokoa.