Bashir kukutana na Salva Kiir

Image caption Bashir anakutana na Kiir kwa mara ya kwanza tangu vita kuanza Disemba 15

Rais wa Sudan Omar al-Bashir anatarajiwa kuwasili mjini Juba kwa mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuhusu mapigano yanayotokota nchini humo.

Vita vimekuwa vikiendelea nchini humo kwa zaidi ya wiki tatu huku pande zinazozozana zikikutana nchini Ethiopia kujaribu kukubaliana juu ya kusitisha vita.

Hadi sasa pande hizo hazijakubaliana chochote.

Mgogoro huo ni kati ya jeshi la serikali ya Rais Kiir na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wake Riek Machar.

Takriban watu 1,000 wameuawa tangu mapigano kuanza tarehe 15 Disemba

Vita vilianza baada ya Rais wa Sudan Kusini kumtuhumu bwana Machar kwa jaribio la mapinduzi, madai aliyoyakanusha.

Takriban watu 200,000 wameachwa bila makao,kutokana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vinavyosemekana kutokana na ukabila.

Aidha Bwana Kiir anatoka kabila la Dinka naye hasimu wake bwana Machar akitoka katika kabila la Nuer.

Vyombo vya habari Sudan Kusini viliripoti kuwa Rais Bashir atakwenda Juba Jumatatu kujadiliana na Rais Kiir kuhusu mzozo huo ingawa hakuna taarifa zaidi zilizotolewa.

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nje mjini Khartoum alisisitiza kuwa Sudan ingependa kuona kipindi salama cha kutafuta mwafaka wa amani Sudan Kusini.

Hadi Ijumaa wiki mwishoni mwa wiki, mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa,Ethiopia, yamekuwa yakiendeshwa na wapatanishi. Lakini sasa pande zinazozozana zinatarajiwa kuanza mazungumzo ya ana kwa ana.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii