Nyota wa Soka Eusebio aaga dunia

Image caption Eusebio miaka alipokuwa kichezea Benfica

Mchezaji soka mashuhuri Eusebio, aliyeingiza mabao mengi zaidi katika kinyang'anyiro cha kombe la dunia mwaka1966, amefariki akiwa na umri wa miaka 71.

Eusebio alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.

Alizaliwa nchini Msumbiji mwaka 1942, wakati ilipokuwa bado koloni ya Ureno. Eusebio da Silva Ferreira alichezea Ureno mara 64 na kuingiza mabao 41.

Mchezaji huyo wa zamani wa Benfica aliingiza mabao tisa katika kombe la dunia la mwaka 1966 nchini Uingereza

Akiwa na sifa ya kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani, aliingiza mabao 733 matika mechi 745 za kulipwa.

Alikuwa amelazwa hospitalini mara kadhaa katika mwaka mmoja uliopita kwa matibabu ya moyo na tatizo la kupumua.

Kadhalika alisifika kwa mchezo wake mzuri sana na hata kutajwa kuwa mchezaji bora zaidi Ulaya mwaka 1965.

Alishinda kombe la Ulaya alipokuwa anachezea Benfica mwaka 1962 na alikuwa miongoni mwa wachezaji walioshindwa na Manchester United katika fainali iliyochezwa Wembly mwaka 1968.

Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji wa kwanza kutoa rambi rambi zao kufuatia kifo cha mchezaji huyo.

Ronaldo anayechezea Real Madrid alisema kupitia ujumbe wake kwa Tiwtter kwamba 'Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.'

Naye mchezaji wa zamani wa Ureno, Luis Figo alisema kwenye Twitter kwamba : "mfalme, tumempoteza mtu mashuhuri sana! "

Mabao ya Eusebio mwaka 1966, yaliisaidia timu yake kuchukua nafasi ya tatu baada ya kushindwa na England kwenye nusu fainali.

Ureno ilishinda mechi zao zote za makundi, huku bingwa watetezi Brazil wakiondolewa katika awamu ya kwanza.

Alipendwa sana na mashabiki wa Uingereza.

Eusebio aliendelea kucheza hadi mwaka 1974, lakini matatizo ya magoti yakaanza kumsumbua.

Baada ya kuacha kucheza soka, alipewa jukumu la kuwa balozi wa soka ya Benfica na Ureno kwa ujumla.