Wahamiaji Waafrika waandamana Israel

Image caption Wahamiaji wa kiafrika nchhini Israel

Maelfu ya wahamijai wa kiafrika, waliandamana mjini Tel Aviv Jumapili kupinga wanavyotendewa na serikali ya Israel.

Waandamanaji hao wengi wao wakiwa raia wa Eritrea na Sudan, wameghadhabishwa na sheria ambazo zinaruhusu kuzuiliwa kwa wahamiaji haramu kwa mwaka mmoja bila ya kufunguliwa mashitaka.

Aidha wanataka kupewa haki ya kufanya kazi huku wakishinikiza serikali kuharakisha maombi yao ya kupewa uraia.

Msemaji mmoja wa serikali alisema kuwa maandamano yao yalifanywa kwa njia ya amani.

"sote ni wakimbizi na ndio tunataka uhuru wala hatutaki kufungwa, '' walisema wahamiaji hao.

Mwandishi wa BBC mjini Jerusalem, Richard Galpin, anasema kuwa maandamano yalichochewa na sheria ya kuwazuilia wahamiaji haramu ambayo iliwaondolea matumaini wengi waliotarajia kuwa serikali ingesitisha kabisa msako dhidi ya wahamiaji haramu.

Wahamiaji hao ambao wengi wamekuwa wakiishi Israel kwa miaka mingi na wanaofanya kazi za kipato cha chini, wanasema wote ni wakimbizi ambao wametoroka nchi zao Eritrea na Sudan kutokana na mateso.

Wanasema kuwa hali yao sasa kutoakana na sheria hiyo watalazimika kuishi jela au kurejea nyumbani.

Kutokana na hatari wanazokabiliwa nazo nyumbani kwao, ina maana kuwa hawawezi kurejeshwa makwao kwa nguvu.

Wahamiaji hao wamesema kuwa watafanya maandamano zaidi nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa na balozi za nchi za kigeni mjini Tel Aviv siku ya Jumatatu.