Kesi dhidi ya Morsi yaahirishwa

Image caption Mohammed Morsi

Taarifa kutoka Misri zinasema kesi dhidi ya kiongozi aliyepinduliwa nchini humo, Mohammed Morsi, imeahirishwa hadi tarehe mosi mwezi Februari.

Jaji anayeendesha kesi hiyo amesema Morsi ameshindwa kuwasili mahakamani leo mjini Cairo kutokana na hali mbaya ya anga.

Lakini mshitakiwa mwenza wa Morsi alisikika akisema kuwa Morsi hawezi kuhudhuria kesi isiyokuwa na uhalali wowote.

Helikopta iliyotarajiwa kumsafirisha hadi katika mji mkuu Cairo anakokabiliwa pamoja na maafisa wengine wa utawala wake na tuhuma za kuchochea mauaji ya waandamanaji mnamo mwaka 2012 alipokuwa madarakani haingeweza kufanya safari hiyo.

Awali vikosi vya usalama viliimarisha ulinzi katika mji mkuu wa Misri Cairo ,Morsi akitarajiwa kuwasili mahakamani.

Yeye na maafisa kadhaa wa serikali yake wanatuhumiwa kwa kosa la kuchochea ghasia na kuwauwa waandamanaji mwaka 2012 wakati wa utawala wake. Mashitaka hayo ni pamoja na kushirikiana na wanamgambo wa kigeni na kuvunja gereza.

Aling'olewa madarakani kwa mapinduzi mwezi julai mwaka jana na kufungwa . Alipofika mahakamani Mwezi Novemba mwaka jana bwana Morsi alisema kuwa bado yeye ni Rais na alifungwa kinyume na matakwa yake

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii