Adhabu kali kwa kuwa na watoto 3 China

Image caption Zhang Yimou ameiomba radhi serikali kwa kosa hilo

Serikali ya China imemtoza faini ya zaidi ya dola milioni moja mtengeza filamu mashuhuri nchini humo, Zhang Yimou kwa kwenda kinyume na sera ya mtoto mmoja kwa kila familia nchini humo.

Bwana Zhang alikiri kuwa na watoto watatu na mkewe na ana hadi siku thelathini kulipa faini hiyo.

Zhang, anayesifika kwa kuendesha sherehe rasmi za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki mwaka 2008, aliomba msahama kwa kukiuka sera hiyo kali.

China ilibuni sera ya mtoto mmoja mapema miaka ya sabini ili kudhibiti ongezeko la watu nchini humo.

Sera hiyo inashurutisha watu wanaoishi mijini kuwa tu na mtoto mmoja, ingawa familia za mashinani ziliruhisiwa kuwa na angalau watoto wawili ikiwa mtoto wao wa kwanza ni msichana.

Lakini mwaka jana, China iliamua kulegeza sera hiyo na kuruhusu familia kuweza kupata watoto wawili ikiwa mzazi mmoja wa mtoto huyo ni mtoto pekee kwao.

Image caption Sera ya mtoto mmoja nchini China ndio imelegezwa tu hivi karibuni

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, bwana Zhang alipata barua kutoka kwa idara ya mpango wa uzazi nchini humo ikimtaka alipe faini.

Faini hiyo ilijumlishwa kulingana na mapato ya bwana Zhang na mkewe Chen Ting, wakati watoto wao wawili walipozaliwa.

Wawili hao walipata mapato ya dola $580,000 mnamo mwaka 2000, 2003 na 2005 kwa mujibu wa serikali.

Mkewe Zhang hata hivyo amekanusha madai kuwa mumewe alipata watoto wengine na wanawake wa kando .

Zhang, mwenye umri wa miaka 61, alitengeza filamu maarufu za China ikiwemo, Hero, The House of Flying Daggers pamoja na The Flowers of War.