Maelfu watoroka Bentiu Sudan Kusini

Image caption Maelfu ya watu wanakimbilia usalama wao kutokana na vita kutokota Sudan Kusini

Ripoti kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa wanajeshi walio watiifu kwa serikali ya rais Salva Kiir wanaendelea kuukaribia mji wa Bentiu unaodhibitiwa na waasi katika eneo lenye utajiri wa mafuta Kaskazini mwa taifa hilo.

Mwandishi wa BBC aliye mjini Bentiu anasema wanajeshi wa serikali wanaaminika kuwa umbali wa kilomita ishirini na tano kutoka mji huo na raia wameingiwa na hofu kubwa.

Maelfu ya watu wanaripotiwa kukimbilia kwenye makao ya jeshi la kulinda amani ya umoja wa mataifa katika mji huo.

Waasi wanaomtii aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar wamekuwa wakiondoshwa kutoka mstari wa mbele wa mapigano.

Mapigano nchini Sudan kusini yalizuka mwezi wa Disemba na mazungumzo ya kuhakikisha mapigano yanakoma hayajazaa matunda.

Takriban Watu 1,000 wameuawa katika mapigano nchini humo na takriban Watu 200,000 wamekimbia mapigano kati ya Jamii ya Dinka na Nuer.

Serikali kadhaa ulimwenguni zimewaondoa Raia wake waliokuwa Sudani kusini, huku Raia wa nchini humo pia wakivuka mipaka kwenda nchi za jirani kutafuta hifadhi.

Mji wa Bentiu ulio kaskazini mwa Sudani kusini ni eneo ambalo lina utajiri wa mafuta.Bentiu na Bor ni miji ambayo inadhibitiwa na Waasi nchini humo.

Mapigano yanayoendelea yamesababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta kwa 20%

Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu limesema kuwa misaada inahitajika kwa wingi nchini Sudani kusini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii