China na Japan zang'ang'ania Afrika

Image caption Shinzo Abe anatarajiwa kuzuru mataifa matatu ya Afrika

China na Japan zimeanza kukosoana kuhusu sera zao barani Afrika huku kila nchi ikiahidi kuongeza kiwango cha cha msaada kwa bara hilo kila mwaka.

Japan imesema kuwa China inawahonga viongozi wa Afrika kwa kuwapa zawadi za kifahari.

Wakati huohuo, China inaituhumu Japan kwa kufanya urafiki na viongozi wa Afrika ili waunge mkono azma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa Japan, Shinzo Abe anazuru mataifa matatu ya Afrika, ikiwa ziara yake ya kwanza barani humo na pia ni ziara ya kwanza ya waziri mkuu wa Japan katika kipindi cha miaka minane.

Bwana Abe anatarajiwa kuahidi msaada wa dola bilioni 14 na pia kutia saini mikataba ya kibiashara nchini Ethiopia, Ivory Coast na Msumbiji.

China kwa upande wake imekuwa ikisifu Afrika kama mahala pa ukelezaji na imeahidi kuongeza msaada wake kwa bara hilo mara dufu hadi dola bilioni 20 kila mwaka.

'Majumba ya kifahari'

Msemaji wa Bwana Abe, Taniguchi anakiri kuwa Japan ingali inajikokota katika uekezaji wake Afrika huku China ikiwa katika msitari wa mbele.

Image caption China ina miradi mingi ya ujenzi Afrika

Lakini aliambia BBC kuwa nchi kama Japan, Uingereza na Ufaransa haziwezi, kuwazawadi viongozi wa Afrika majumba ya kifahari ili kupata nafasi za uekezaji.

China wakati mwingi, hukubali kugharamia ujenzi wa majengo ya serikali mfano makao makuu ya Muungano wa Afrika ambako Abe anatarajiwa kutoa hotuba yake siku ya Jumanne.

Bwana Taniguchi alikariri kwamba , sera ya Japan kuhusu Afrika, ni kusaidia maendeleo ya wananchi na kukuza vipaji pamoja na kutoa mafunzo ya kiteknolojia.

Wakati huohuo China inasisitiza kwamba ushirikiano wake na Afrika ni wa kujitolea.

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi aliambia jarida moja mjini Hong Kong kwamba China haiwezi kukubali jambo la baadhi ya mataifa yanayo jaribu kushindana na nchi zengine kwa maslahi yao wenyewe na kutoa msaada kwa Afrika kwa sababu za kisiasa pekee.

Bila shaka kauli hii ililenga Japan kwa juhudi zake za kutaka kushawishi mataifa ya Afrika kuunga mkono hatua yake ya kutaka kuwa mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jambo ambalo China inapinga vikali. Nani mkweli kati ya Japan na China? toa maoni yako kwenye ukurasa wetu wa facebook bbcswahili