Kizungumkuti cha mapatano Sudan Kusini

Image caption Maelfu ya watu wameachwa bila makao baadhi wakikimbilia katika nchi jirani

Mazungumzo ya kupatanisha pande zinazozozana katika mgogoro wa Sudan Kusini, yameendelea kukwama huku kiongozi wa waasi Riek Machar akikataa kutia saini mkataba wa kusitisha vita hadi wafungwa 11 wa kisiasa watakapoachiliwa.

Wapatanishi wa IGAD pamoja na wajumbe wa kimataifa kutoka Marekani , Uingereza na Norway, walikutana na waasi kujaribu kuwashawishi kusitisha vita.

Wapatanishi hao wamerjea mjini Addis Ababa, Ethiopia ambako mazungumzo yanatarajiwa kuanza tena.

Wakati huohuo, wanajeshi wa serikali Nchini Sudan Kusini wameanza kuelekea katika mji wa Bor ambao ndio wa mwisho unaodhibitiwa na waasi.

Msemaji wa jeshi Kanal Phillip Aguer, ameelezea kuwa Bor ungali mikononi mwa waasi lakini wanajeshi wa serikali wanaelekea katika mji huo.

Mji wa Bor uko umbali wa kilomita 200 Kaskazini mwa Juba.

Mapigano nchini Sudan Kusini ni kati ya waasi na wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir, wanajeshi waasi na makundi ya wapiganaji wa kikabila ambao wanaongozwa na Riek Machar, makamu wa zamani wa Rais chini ya serikali ya Kiir.

Wanajeshi wa serikali walikomboa mji muhimu wa Bentiu wiki jana lakini makabiliano kadhaa yameshuhudiwa katika sehemu moja iliyo umbali wa kilomita 20 kutoka mji wa Juba.

"Rais Salva Kiir amelima kikosi kikubwa cha wanajeshi kushambulia waasi hao ambao walishinda baada ya vita vya karibu masaa mawili.

Kanali Aguer alithibitisha kuwa makabiliano yalitokea lakini hapakuwa na taarifa za kuthibitisha nani aliyeshinda vita hivyo.

Waasi hao wanaongozwa na mpiganji anayesifika sana Alfred Ladu Gore ambaye ni mmoja wa watu wanaosakwa na serikali ya Rais Kiir.

Waasi nao wanadai kuwa wanakaribia kuuteka mji wa Malakal,ambao ni mji mkuu wa jimbo la Upper Nile unaozalisha mafuta.