Wanajeshi waasi warejea kazini CAR

Image caption Wanajeshi walioasi walifanya hivyo kwa kuhofia mashambulizi

Mamia ya wanajeshi walioasi jeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,wameanza tena kurejea kazini katika mji mkuu wa Bangui.

Wengi walioasi walikuwa Wakristo waliohofia kuwa huenda wakashambuliwa na wenzao waisilamu baada ya mapinduzi ya mwaka uliopita yaliyoongozwa na Waislamu wengi waasi wa kundi la Seleka.

Baadhi ya wanajeshi hao walikuwa wamejiunga na wanamgambo wa kikristo.

Taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati, limekumbwa na mapigano ya kidini kwa karibu mwaka mmoja sasa lakini Rais wa mpito wa sasa, Alexandre-Ferdinand Nguendet, ametangaza kuwa wakati wa ghasia umefika kikomo nchini humo.

Alisema kuwa amewaonya waasi na waporaji kuwa wakati wao wa kusherehekea vya bure umekamilika.

Hata hivyo BBC imepokea habari za kusikitisha ambapo mkaazi mmoja wa Bangui alionekana akila nyama ya Mwislamu aliyekuwa ameuliwa na umma.