Mchakato wa katiba mpya Misri

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hali ya usalama imedhibitiwa vikali wananchi wakijitokeza kupigia kura ya maamuzi katiba mpya

Watu nchini Misri wameanza kupigia kura ya maamuzi rasimu ya katiba mpya huku hali ya usalama ikiwa imedhibitiwa vikali.

Katiba mpya ndio itatoa njia kwa uchaguzi mkuu mpya kufanyika.

Madhumuni ya katiba hiyo mpya ni kutupilia mbali katiba ya zamani iliyopitishwa na iliyokuwa serikali ya Mohammed Morsi miezi kadhaa kabla ya jeshi kumuondoa mamlakani.

Jeshi linataka watu waipigie kura ya Ndio katiba hiyo ambayo ndiyo ishara ya kuondoka kabisa kwa Morsi ambaye wafuasi wake wamekuwa wakisema ni rais halali wa Misri.

Vuguvugu la Muslim Brotherhood ambalo sasa limetajwa kuwa kundi la kigaidi linasusia uchaguzi huo. Pia ghasia zimeripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Kupinduliwa kwa serikali ya Hosni Mubarak hadi sasa hakujaleta mabadiliko ya kidemokrasia kama ilivyokusudiwa nchini Misri.

Hata hivyo baada ya mapinduzi hayo, kumekuwa na nafasi ya kupiga kura kwa mabadiliko fulani. Hii ni mara ya tatu katika muda wa miaka mitatu kwa Wamisri kupiga kura ya maamuzi.

Matokeo mawili ya kwanza yalitupiliwa mbali kufuatia wimbi la ghasia za kisiasa. Serikali ya mpito inayoungwa mkono na jeshi, inasema kuwa licha ya matatizo fulani kutarajiwa mambo yatakuwa tofauti mara hii.

Kuna taarifa kuwa wapinzani wametiwa mbaroni kwa madai ya kuweka mabango yanayopinga katiba.

Rasimu hiyo bado inaipa jeshi mamlaka makubwa ikiwemo jukumu la kumteua waziri wa ulinzi, kwa ajili ya kutetea bajeti ya jeshi na kufikisha raia katika mahakama za kijeshi.

Ikiwa katiba hii itaidhinishwa, basi itakuwa ishara ya kuunga mkono mapinduzi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia