Shambulizi la kujitoa mhanga Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jeshi la Serikali limekuwa likipambana na Boko Haram imekuwa vigumu kuliangamiza

Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari moja limelipuka mjini Maiduguri Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na kuna hofu watu wengi wamejeruhiwa.

Majeruhi walionekana wakitoroka eneo la shambulizi ambalo lilikuwa na uharibifu mkubwa, huku wanajeshi wakifyatua risasi hewani.

Duru zinaarifu kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga ndiye aliyesababaisha shambulizi hilo lililotokea karibu na soko rasmi.

Kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram, limekuwa likihusika na mashambulizi kadha wa kadha katika eneo hilo ambalo ni kitovu cha kundi hilo.

Boko Haram linatumia ghasia na mauaji kushinikiza serikali kuidhinisha sheria za kiisilamu kutumika Kaskazini mwa Nigeria.

Jeshi limethibitisha BBC kutokea kwa mlipuko huo, lakini halikuweza kueleza idadi ya walioathirika.

Mtu mmoja aliyeshuhudia shambulizi hilo amesema ameona miili ya baadhi ya waliouawa kwenye shambulizi hilo ikiwa imetapakaa ardhini.

Gari la pili lililokuwa limeegeshwa kando ya gari lililolipuka liliteketea kutokana na mlipuko huo.