Kitendawili cha jeshi la UG S.Kusini

Image caption Waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya Rais Kiir wanaongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar

Wabunge nchini Uganda leo wanaanza kujadili hatua ya serikali kuwapeleka bila idhini ya bunge wanajeshi wa taifa hilo nchini Sudan Kusini.

Serikali iliamrisha wanajeshi hao kupelekwa Sudan Kusini kufuatia mapigano yaliyozuka huko Disemba mwaka jana.

Mjadala unatarajiwa kuwa mkali kwani baadhi ya wabunge wanahoji uhalali wa majeshi ya Uganda kuwepo nchini Sudan Kusini.

Jukumu la wanajeshi hao katika vita hivyo bado halijawekwa wazi kwa wabunge watakaopigia kura hoja hiyo.

Waziri wa ulinzi anatarajiwa kuhojiwa kuhusu swala hilo kabla ya wabunge kupiga kura kuidhinisha wanajeshi hao kushika doria Sudan Kusini.

Rais Yoweri Museveni alisikika akitoa vitisho dhidi ya kiongozi wa waasi Riek Machar kuwa ikiwa hatasitisha vita huenda akapeleka wanajeshi wa Uganda kwenda kusaidia majeshi ya serikali ya Sudan Kusini kupambana na wapiganaji wake.

Museveni aliamrisha majeshi hayo kwenda Uganda wakati wabunge walipokuwa likizoni, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wabunge hao.

Jumanne waziri wa ulinzi atatakiwa kufafanua na kutoa majibu kuhusu muda ambao wanajeshi wa Uganda wataendelea kusalia Uganda pamoja na kutaka kujua kazi wanayoifanya huko.

Baadhi ya wabunge wamemtuhumu Rais Yoweri Museveni kwa kwenda kinyume na katiba kwa kuwaamrisha wanajeshi wa nchi kwenda Uganda kuwaokoa raia waliokuwa katika nchi hiyo inayokumbwa na mgogoro wa kisiasa wakati vita vilipozuka.

Wabunge hao wanahoji Wanajeshi wa Uganda wako Sudan Kusini kwa mwaliko wa nani, ikiwa ni IGAD au AU wanataka kujua.

Wanaituhumu serikali kwa kukosa kutoa majibu kuhusu idadi ya wanajeshi wa UDF walio nchini humo wakihofu hali ya usalama.