Israel yamuomba radhi Kerry

Haki miliki ya picha AP
Image caption Israel imesikitika na kumuomba radhi Kerry kwa matamshi ya bwana Yaalon

Waziri wa ulinzi wa Israel Moshe Yaalon ameomba radhi kwa matamshi yake yaliyochapishwa katika gazeti moja nchini humo, ya kumhujumu waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuhusu anavyoshughulikia mzozo wa Mashariki ya kati.

Bwana Yaalon alinukuliwa akisema kuwa bwana Kerry ana 'hamasa kubwa kupindukia'na anajiona kama yeye ndiye 'mwokozi wa mchakato' wa amani Mashariki ya Kati.

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani imeelezea kughadhabishwa na matamshi hayo.

Hata hivyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, bwana Yaalon amesema kuwa hakuwa na nia yoyote ya kumkosea heshima Kerry.

"Waziri wa ulinzi anaomba radhi ikiwa matamshi yake yamemuudhi bwana Kerry.’’

“Marekani na Israel zina lengo moja la kuendelea na mazungumzo na wapalestina,’’ ilisema taarifa hiyo.

"Tunamshukuru Kerry kwa juhudi zake kubwa kutafuta mwafaka wa Amani.’’

Ikulu ya White house imesema kwamba matamshi ya Israel hayafai kabisa ikizingatiwa kuwa Marekani inasaidia Israel kiuasalama.