Uharamia umetokomezwa Somalia?

Image caption Mkondo wa uharamia katika bahari hindi

Uharamia katika pwani ya Somalia umepungua sana katika miaka sita iliyopita.

Ni visa 264 vya utekaji meli pekee vimeripotiwa.

Wataalamu wanasema uharamia umeshuka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2011.

Mwaka jana ni visa 15 pekee vya meli kutekwa vilivyoripotiwa, kwa mujibu wa shirika la kimataifa la safari za baharini IBM.

Shirika hilo linasema kuwa visa hivyo vimeshuka kutoka 75 mwaka 2012 na 237 mnamo mwaka 2011.

Walinzi waliojihami, manowari za kijeshi zinazoshika doria na uthabiti wa serikali ya Somalia ni miongoni mwa mambo yaliyochangia , kupungua kwa visa vya uharamia.

Ripoti ya shirika hilo, inasema kuwa zaidi ya watu 300 walitekwa nyara mwaka 2013 huku wengine 21 wakijeruhiwa kwa risasi na visu.

Indonesia ndio iliathirika zaidi na uharamia mwaka jana ikiwa ni asilimia hamsini ya visa vyote vya uharamia vilivyoripotiwa duniani.

Katika kanda ya Afrika Magharibi, ni asilimia 19 pekee ya visa vya uharamia viliripotiwa.

Maharamia nchini Nigeria walitumia nguvu wakati wa mashambulizi yao wakati mwingine hata wakiwaua waathiriwa na kuwateka nyara watu 36.

Mwezi Novemba, ripoti ya Umoja wa Mataifa na benki ya dunia, ilisema kuwa maharamia katika ufuo wa pwani ya Somalia, walipata dola milioni 400 pesa zilizotolewa kama kikombozi kati ya mwaka 2005 na 2012.