Mjukuu wa Mandela matatani

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mandla ni mjukuu wa kwanza wa Hayati Nelson Mandela

Mjukuu wa hayati Nelson Mandela, Mandla Mandela , ameshitakiwa kwa kosa la kumshambulia mtu na kumtisha kwa bunduki.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari nchini Afrika Kusini.

Inadaiwa Mandla, alimshambulia mwalimu, Mlamli Ngudle na hata kumtisha kwa bunduki baada ya Mwalimu huyo kuligonga gari la mmoja wa marafiki zake mwaka jana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari tarehe 24 baada ya kusikilizwa kwa muda katika mahakama ya Mthatha.

Mandla alirithi wadhifa wa babu yake kama kiongozi wa kitamaduni.

Mwendesha mkuu wa mashitaka aliwasilisha mahakamani mashitaka mawili dhidi ya Mandla,la kwanza likiwa kumshambulia mtu na pili kumtisha kwa silaha.

Bado hajasema ikiwa anakiri au kukanusha mashitaka hayo lakini wakili wake aliitaka mahakama kuahirisha kesi dhidi yake akisema kuwa alipokea mashitaka hayo leo tu na kuwa anahitaji muda zaidi kuyatathmini.

Bwana Mandela ni kiongozi wa kijamii katika kijiji cha Mvezo,ambako babu yake alizaliwa.

Mandla amekuwa kwenye mvutano na shangazi yake Makaziwe kila mmoja akitaka kutambuliwa kama kiongozi wa familia ya Mandela.

Ni mjukuu wa kwanza wa Mandela wakati Makaziwe ni mtoto wa kwanza wa hayati mzee Mandela.