Kashfa ya Hollande imedumu miaka 2

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hollande na mpenzi wake rasmi Valerie Trierweiler

Jarida la udaku nchini Ufaransa ambalo lilichapisha taarifa za Rais wa nchi hiyo Francois Hollande kuwa na mpenzi wa kando, limedai kwamba Hollande amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Muigizaji Julie Gayet kwa miaka miwili.

Jarida hilo pia limechapisha picha zaidi za Hollande na Bi Gayet wakiwa pamoja.

Gayet amesema kuwa atawashitaki wahariri wa jarida hilo kwa kuingilia maisha yake.

Mpenzi rasmi wa Rais Hollande Valerie Trierweiler, angali hospitalini ambako alilazwa baada ya kupata taarifa za kashfa ya mapenzi ya Hollande wiki moja iliyopita.

Jarida hilo limesema kuwa Rais Hollande alikuwa na nyumba nyingine ambako alikuwa anakutania na Gayet mjini Paris.

Inadaiwa kuwa wawili hao walikuwa pamoja nyakati za wikendi Kusini mwa Ufaransa na kwamba Hollande alipata kisibabu cha kutosafiri na mpenzi wake Trierweiler kwenda Ugiriki,ili aweze kuwa na Gayet.

Bi Gayet amelishitaki jarida hilo akitaka kulipwa dola 68,000 kwa kuingilia maisha yake ya faragha.

Ikiwa atashinda kesi hiyo ,jarida la Closer litahitajika kuchapisha uamuzi wa mahakama katika kurasa za mbele za jarida hilo.

Hata hivyo bwana Hollande aliamua kutolichukulia hatua za kisehria jarida hilo hata baada ya kutishia kufanya hivyo.

Picha za jarida hilo zimeleta msukosuko katika serikali ya Rais Hollande