Iran nje ya mkutano wa Syria-UN

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amefutilia mbali mwaliko uliotolewa kwa Iran kuhudhuria mazungumzo ya amani ya Syria nchini Uswizi.

Msemaji wa Ban Ki Moon, alisema Katibu Mkuu huyo alichukua uamuzi huo kwa sababu Iran, ilikataa kutoa ahadi ya wazi kwamba inaelewa na inaunga mkono hatua ya kuundwa kwa serikali ya mpito Syria, licha ya kutoa ahadi zisizo rasmi kuhusu hilo.

Umoja wa Mataifa umelazimika kufutilia mbali mwaliko wake kwa Iran uliokuwa umeitaka nchi hiyo kuhudhuria kongamano linalonuiwa kutafuta Amani ya Syria.

Sababu kuu ni kwamba Iran, ilikataa kuunga mkono pendekezo la kuwa na seriali ya mpito nchini Syria.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky amedokeza kuwa Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesikitishwa sana na uamuzi huo wa Iran uliokataa pendekezo la serikali ya mpito ambalo liliafikiwa na jumuiya ya kimataifa hapo 2012 kama njia moja ya kutafuta dawa ya mzozo wa Syria.

Lakini kwamba kikao hicho cha Amani ya Syria kitaendelea bila Iran, si ajabu Ban ki-Moon ndie aliyewashangaza wengi pale alipopeleka mwaliko huo kwa Iran na kusababisha mzozo wa kidiplomasia.

Wapinzani wa serikali ya Syria walikasirika na kutishia kutohudhurua kikao hicho.

Marekanii kwa upande wake ilikuwa tayari kushinikiza kuwa iwapo Iran haitakubali pendekezo la serikali ya mpito ya Syria basi isialikwe.

Huku malumbano hayo yakiendelea Iran ilikuwa imetangaza kujioindoa.

Balozi wa Iran katika umoja wa Mataifa Mohammad Khazaee, amenukululiwa akisema Iran, inataka sana suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Syria lakini haitakubali masharti kama kigezo cha kushiriki mazungumzo hayo ya amani.