Sudan Kusini yakataa matakwa ya waasi

Image caption Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr

Mkutano wa rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na waandishi umefanyika huku serikali ikitoa kauli kuwa imefanikiwa kuunyakua mji wa Malakal, makao makuu ya jimbo la Upper Nile.

Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na viongozi wa waasi wanakoshiriki mazungumzo ya amani nchini Ethiopia.

Rais Kiir ameeleza kuwa anataka usitishwaji wa mapigano usiokuwa na masharti na kusisitiza kuwa hatawaachilia huru washirika wa karibu kumi na mmoja wa aliyekuwa makamu wake Riek Machar walioko kizuizini, moja wapo ya madai muhimu ya kiongozi huyo wa waasi, Riek Machar.

"La kwanza, tunataka kukomeshwa kwa uhasama na mapigano pasipo masharti miongoni mwa pande zinazohasimiana hapa nchini, haraka iwezekanavyo". Alisema rais Kirr.

Machar amesema hatasaini mkataba wa amani kabla majeshi ya Uganda yanayopigana bega kwa bega na majeshi ya serikali kuwang'oa waasi hayajaondolewa kutoka Sudan Kusini.

Rais Kiir ametoa wito kwa mpinzani wake na kundi lake kujifunza kutotumia nguvu kuchukua madaraka, na kuongeza kuwa serikali yake bado ina nafasi moyoni kumsamehe Machar.

Kiongozi huyo wa Sudan Kusini ambaye sasa anaonekana kupata nguvu mpya baada ya machafuko ya mwezi mzima, amesema serikali yake inapanga maandalizi kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani, endapo amani itarejea.