UN: Hatujahusika na vita S. Kusini

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maelfu ya watu waliotoroka vita wanahifadhiwa katika kambi ya jeshi Sudan Kusini

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amekosoa kikosi cha Umoja wa mataifa cha kulinda amani nchini humo (UNMISS) kwa kujihusisha na vita vya nchi hiyo.

Rais Kiir amesema kuwa kikosi hicho kimejipa cheo cha kutawala nchi hiyo kama serikali mbadala.

Pia amekituhumu kikosi hicho pamoja na mashirika mengine ya misaada kwa kuunga mkono waasi na kuwapa maficho katika makao yao ambako wakimbizi wa ndani wamepewa hifadhi.

Zaidi ya watu 70,000 wanahifadhiwa katika kambi za jeshi la Umoja wa Mataifa kutokana na vita vilivyozuka mwishoni mwa mwaka jana.

Msemaji wa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa Ariane Quentier amekanusha madai kuwa jeshi la Umoja wa Mataifa linaingilia siasa za nchini humo.

Aliambia BBC kuwa wanahifadhi wakimbizi wa ndani waliotoroka vita na ambao wanahofia kurejea makwako kwani hali bado ni tete.

''Tulikuwa na wakimbizi wa ndani elfu sabini waliohisi kuwa mahala walipokuwa wanaishi sio salama na kutafuta usalama hapa. Wengi wa wakimbizi hawa ni wanawake na watoto ambao bila shaka sio waasi,'' alisema Quentier

Wakati huohuo, Rais Kiir, amesema kuwa jeshi lake limeinyakua miji ya Bentiu, Bor na Malakal kutoka mikononi mwa waasi.

Lakini waasi wameieleza BBC kuwa bado wanadhibiti Malakal, ambao ni mji muhimu kuelekea visima vya mafuta katika jimbo la Upper Nile.

Kwingineko mazungumzo ya kumaliza mapigano nchini Sudan Kusini yangali yanaendelea nchini Ethiopia