Mazungumzo ya Syria yaanza rasmi Geneva

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa na mjumbe wake nchini Syria Brahimi

Siku ya kwanza ya mazungumzo rasmi ya amani kati ya serikali ya Syria na waasi yanatarajiwa kuanza mjini Geneva.

Siku ya Alhamisi, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi, alifanya mashauriano ya pande hizo mbili ili kutathmini ikiwa wako tayari kufanya mazungumzo ya pamoja.

Uswizi ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo kwa siku ya kwanza mjini Montreux, ambapo wajumbe wa pande hizo mbili walirushiana maneno makali.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu laki moja wameuawa nchini Syria Tangu mzozo huo kuanza miaka mitatu iliyopita.

Mapigano hayo pia yamesababisha zaidi ya watu milioni tisa nukta tano kuhama kutoka makwao, hali iliyosababisha hali mbaya ya kibinadam ndani ya nchi hiyo na pia katika nchi jirani.

Brahimi alifanya mazungumzo tofauti ya faragha na waakilishi wa rais Bashar al-Assad na wale wa baraza la mpito.

Muda wa mazungumzo haijulikani

Haki miliki ya picha b
Image caption Rais Bashar akishauriana kuhusu mzozo unaokumba taifa lake

Mazungumzo hayo hayakutarajiwa kufanyika kwani pande hizo mbili hazikuwa zimekutana kufanya mashauriano yoyote rasmi.

Mabalozi wa mataifa ya Magharibi wanasema, wasi wasi mkuu wa Bwana Brahimi, wakati wa mazungumzo hayo siku ya Ijumaa, ni kuhakikisha kuwa hakuna pande ambayo itaondoka na kususia mazungumzo hayo.

Hata hivyo wajumbe hao hawatarajiwi kushauriana moja kwa moja baada ya kufanya kikao cha pamoja na bwana Brahimi, ripoti zinasema kuwa watapewa vyumba tofauti ili kujadiliana wenyewe kabla ya kuwasilisha mapendekezo yao.

Haijulikani mazungumzo hayo yataendelea hadi lini na wajumbe hao wanatarajiwa kupanga ratiba yake.

Serikali ya Syria inatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kupambana na ugaidi huku upinzani ukiweka agenda kuu kuwa kuondolewa kwa rais Bashar al-Assad.

Kiongozi wa Muungano wa Baraza la Kitaifa, Ahmed Jarba amewaambia waandishi wa habari kuwa, jamii ya kimataifa kwa sasa imeridhika kuwa rais Assad hatasalia madarakani kwa muda mrefu ujao.