Vitisho kwenye mkutano wa Syria Geneva

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mamilioni ya watu wameachwa bila makao kutokana na vita nchini Syria

Waakilishi wa serikali ya Syria katika mazungumzo ya amani kati ya wanaharakati na serikali, wametishia kuondoka kwenye mazungumzo hayo ya amani ikiwa mazungumzo muhimu hayatakuwa yameanza ifikapo Jumamosi.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Muallem, ametoa tisho la kujiondoa kwenye mazungumzo baada ya kukutana na mjumbe maalum wa UN nchini Syria Lakhdar Brahimi.

Bwana Brahimi anatarajiwa kukutana na upande wa upinzani baadaye Ijumaa.

Duru zinasema kuwa mazungumzo yamekumbwa na changamoto hasa kwa kuwa pande zote mbili zina misimamo mikali.

Mgogoro wa kisiasa nchini Syria, umesababisha vifo vya watu 100,000 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Ghasia hizo pia zimesababisha watu milioni 9.5 kutoroka makwao, na kusababisha hali mbaya ya kibinadamu ndani ya Syria na katika nchi jirani.

Hii ni siku ya tatu ya mazungumzo mjini Geneva lakini mkutano wa kwanza rasmi ambapo mazungumzo yanaanza.

Kulikuwa na matumaini ya mkutano wa ana kwa ana kati ya serikali na wanaharakati, lakini baadaye bwana Brahimi alifanya mazungumzo na kila upande.

Pande hizo zinalaumiana kwa changamoto hiyo.