Al-Sisi kuwania Urais Misri

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkuu wa jeshi Misri Abdel Fattah Al-Sisi

Viongozi wa kijeshi nchini Misri wamekubaliana Mkuu wa jeshi ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi Abdel Fattah Al Sisi kuwania Urais katika Uchaguzi unaotarajiwa miezi michache ijayo.

Field-Marshal al-Sisi anatarajiwa kujiuzulu kutoka jeshini na kutangaza azma yake ya kuwania urais siku chache zijazo.

Waandishi wa habari wamesema mwanajeshi huyo anapigiwa upatu kushinda kwa urahisi katika uchaguzi unaotarajiwa hapo Aprili ambapo hana upinzani mkubwa.

Al Sisi anaaminika kuchangia pakubwa katika kumuondoa madarakani Rais Mohammed Mosri mwaka jana kufuatia maandamano makubwa dhidi yake.

Mikutano ya hadhara ilifanyika wikendi hii huku kukiwa na wito wa kumtaka Bw. Al Sisi kuwania Urais.

Binafsi Al Sisi hajatangaza kugombea lakini kumekua na taarifa kwamba alikua akijitayarisha kujitosa katika kinyang'anyiro cha kuongoza Misri.

Maelfu ya raia walikusanyika katika medani ya Tahiri hapo Jumamosi na kumtaka mkuu wa jeshi kuwania Urais.

Hapo Jumapili Kaimu Rais Adly Mansur alitangaza kwamba uchaguzi wa Rais utafanyika kabla ya kuwachagua wabunge. Wadadisi waliona tangazo hilo kama kumpa nafasi Al Sisi kugombea Urais. Wafuasi wake wamesema Misri inahitaji kiongozi mkali kama yeye.

Kwa sasa dalili zote ni kwamba Mkuu huyo wa jeshi atashinda kwa urahisi. Hata hivyo wapinzani wake wanaonya huenda Misri ikarejea katika utawala wa kiimla ambao uliondolewa na maandamano ya raia miaka mitatu iliyopita.