Taharuki kuhusu neno 'Allah' Malaysia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji wakipinga wakristo kutumia neno 'Allah'

Polisi nchini Malaysia wanasema kuwa wamedhibiti ulinzi wa makanisa katika jimbo la Penang baada ya moja ya makanisa kushambuliwa kwa mabomu.

Shambulizi hilo limezua wasiwasi kuhusu kuibuka hali ya taharuki kati ya waisilamu walio wengi na wakristo kukithiri kutokana na matumizi ya neno "Allah" miongoni mwa wakristo.

Mabango yaliyokuwa na maandishi '' Allah ni mkubwa, Yesu ni mwana wa Allah'' yalipatikana yakiwa yamewekwa nje ya makanisa matatu katika jimbo la Penang,ikiwemo kanisa moja lililoshambuliwa.

Viongozi wa kanisa wanakanusha madai kuwa wao ndio walioweka mabango hayo, lakini mashambulizi hayo yanaonekana kuwa ya kulipiza kisasi.

Oktoba mwaka jana, ni waisilamu pekee wanaotumia neno Allah kumaanisha Mungu. Wakristo wa asili ya Borneo nchini Malaysia wanasema kuwa wamekuwa wakitumia neno Allah kwa karne nyingi.