Wakamatwa na pembe za Ndovu Togo

Image caption Afrika inakabiliana na changamoto ya kutokomeza biashara haramu ya pembe za Ndovu

Polisi nchini Togo wamewakamata watu watatu baada ya kuwanasa na tani mbili za pembe za Ndovu wakizafirisha kwenda Vietnam

Wawili kati ya washukiwa hao ni raia wa Togo na mwengine ni raia wa Vietnam.

Watetezi wa mazingira, Magharibi mwa Afrika wanasema kuwa eneo hilo, ni kitovu cha kusafirishia pembe za Ndovu kutoka Afrika ya Kati hadi Asia.

Licha ya marufuku ya biashara ya Pembe za Ndovu, karibu nusu karne iliyopita, idadi ya Ndovu wa Afrika inaendelea kupungua na huenda wakatokomea.

Idadi ya Ndovu hao imepungua kwa asilimia 60 katika miaka kumi iliyopita.

Pembe hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya Konteina pamoja na mbao ambazo zilikuwa zikisafirishwa kwenda Vietnam.

Watetezi wa mazingira wanasema kuwa kiwango cha pembe hizo kinaonyesha kama ni Ndovu 230 waliuawa.

Mataifa ya Afrika yanakabiliana na changamoto ya kukomesha biashara haramu ya Pembe

Siku ya Jumanne mahakama moja nchini Kenya ilitumia kwa mara ya kwanza sheria zake kali za kupambana na biashara haramu ya pembe za Ndovu kwa kumtoza mchina mmoja faini ya dola zaidi ya laki mbili.

Alikamatwa wiki jana akiwa na kilo tatu na nusu za pembe za ndovu katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi