AU kuzungumzia migogoro Afrika

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma

Viongozi wa Afrika wameanza mkutano wao katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa ambapo agenda yao kuu itakuwa swala la mizozo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa tume ya Umoja huo Nkosazana-Dlamini Zuma amewaambia viongozi 54 ambao ni wanachama wa Muungano wa Afrika, kwamba wanapaswa kushirikiana ili kuleta suluhu ya kudumu kwa migogoro Afrika.

Jamhuri ya Afrika ya kati imekumbwa na mgogoro wa kisisa kwa miezi kumi sasa tangu waasi kuipindua serikali.

Katika taifa jirani ya Sudan Kusini, makundi hasimu yalitia saini ya mapatano juma lililopita baada ya mapigano makali yaliyodumu mwezi mmoja, lakini mapigano yangali yanatokota kati ya serikali na waasi.

Maelfu ya watu wameuwawa katika mzozo huo.

Mkutano huo pia utaangazia,tatizo la uhaba wa chakula na kilimo katika bara hilo. Licha ya uchumi kukuwa katika sehemu nyingi za Afrika,eneo la Sahel na upembe wa Afrika ni maeneo ambayo hukumbwa na tatizo la uhaba wa chakula mara kwa mara.

Muungano wa Afrika umekosolewa kwa kujikokota katika kuchukua hatua kukabiliana na migogoro ya kisiasa Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Muungano huo umemteua Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz kama mwenyekiti wake mpya.

Generali Abdel Aziz aliingia mamlakani nchini Mauritania mwaka 2009, baada ya kuongoza matukio mawili ya mapinduzi katika kipindi cha miaka minne.