'Wapinzani' wabomolewa nyumba Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waathiriwa wa vita nchini Syria

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeishutumu serikali ya Syria kwa kubomoa maelfu ya nyumba za watu kama njia ya kuwapa adhabu wananchi wanaoshukiwa kuwaunga mkono waasi dhidi ya Rais Assad.

Shirika hilo limetoa picha za Satelite kama ushahidi wa kuthibitisha madai yao.

Ripoti hiyo ilisema kuwa ushahidi wa picha,video na picha za satelite, pamoja na ushahidi kutoka kwa waathiriwa,umeonyesha kuwa serikali ya Syria, iliharibu kwa maksudi nyumba za watu kinyume na sheria za vita.

Imesemekana hakuna sababu iliyotolewa na jeshi ya kubomolewa kwa nyumba hizo kwani washukiwa wangeadhibiwa tu ikiwa kuna makosa yoyote waliyafanya.

Picha za satellite zilionyesha uharibifu mkubwa wa nyumba na makazi ya watu viungani mwa mji wa Damascus na nyingine katika mji wa Hama ambako inaaminiwa kijiji kizima kiliharibiwa.

Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa uharibifu ulifanyika bila onyo lolote wala malipo kwa wathiriwa na kuwa maelfu ya familia zimeachwa bila makao.

Kadhalika shirika hilo lilipuuzilia mbali taarifa kutoka kwa maafisa wa serikali kuwa nyumba zilibomolewa kwa sababu ya mipangilio mipya ya mji au kwa sababu zilijengwa kinyume na sheria.

Shirika hilo limetoa wito kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuishitaki Syria kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita wito ambao umeungwa mkono na upinzani nchini Syria.

Hata hivyo hilo huenda lisifanyike kwani kutahitajika kuwepo makubaliano ya pamoja katika baraza hilo, jambao ambalo huenda lisiwezekane kwani Urusi na China zimekuwa zikiunga mkono Syria.