Usalama wadhibitiwa Afrika Mashariki

Image caption Al Shabaab walishambulia Kenya mwaka jana na kusababisha maafa

Hali ya usalama nchini Kenya imedhibitiwa vikali kufuatia tisho kutoka kwa kundi la wanamgambo wa kiisilamu wa Al Shabaab kushambulia nchi zinazounga mkono serikali ya Somalia katika vita dhidi ya wanamgambo hao.

Kundi hilo limesema linalenga nchi ambazo zimetuma wanajeshi wao nchini Somalia kusaidia serikali ya nchi hiyo kupambana nao.

Wasafiri katika uwanja wa kimataifa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi , wametatizika baada ya maafisa wa usalama kudbibiti hali ya usalama hasa kwa watu wanaoingia katika uwanja huo.

Wasafiri wanalazimika kupanga foleni ndefu huku wakikaguliwa kwa masaa. Kadhalika polisi wameanza kuwasaka raia wa kigeni wasio na vyeti halali vya kuwa nchini Kenya.

Miongoni mwa waliokamatwa ni mwanadiplomasia mmoja mwenye uraia wa kisomali.

Sio nchini Kenya tu ambako hali ya usalama imedhibitiwa. Kanda ya Afrika Mashariki yote iko katika hali ya tahadhari, baada ya kundi hilo kutishia kushambulia nchi zinazounga juhudu dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab nchini Somalia.

Balozi za kimataifa zimetaja viwanja vye ndege, majengo ya serikali na maeneo ya umma kuwa miongoni mwa maslahi ambayo huenda yakashambuliwa.

Tahadhari hiyo imetolewa kwa Kenya, Somalia na Ethiopia na inakuja baada ya kifo cha wapiganaji wa kundi la al shabaab nchini Somalia pamoja na kuuawa kwa mtu aliyeshukiwa kuwa gaidi nchini Kenya.

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab lilishambulia jengo la Westgate mwaka jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya sitini.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imesema kuwa usalama umedhibitiwa vikali katika majengo ya serikali.

Maafisa nchini Ethiopia pia wamedhibiti usalama. Uganda, Burundi na Kenya ni baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zilizo na wanajeshi wao nchini Somalia.