UN:Milioni 3.7 wana njaa S.Kusini

Haki miliki ya picha Getty
Image caption UN inasema kuwa vita vinaendelea licha ya mkataba wa amani kutiwa saini

Umoja wa mataifa unakadiria kwamba takriban watu millioni 3.7 nchini Sudan kusini wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi walio watiifu kwa aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar.

Mratibu wa maswala ya kibinaadamu katika umoja huo Toby Lanzer ameiambia BBC kwamba mzozo huo ulioanza mwezi Disemba mwaka jana umeharibu masoko pamoja na maisha ya kawaida ya watu, mbali na kusababisha hali mbaya ya kibinaadamu kwa thuluthi moja ya idadi ya raia.

Na ili kuzuia Janga ,amesema kuwa umoja wa mataifa unahitaji dola millioni 1.3 pamoja na mazingira yalio salama ili kutekeleza wajibu wake.

Maelfu ya raia wamepoteza maisha yao katika vita hivyo ambavyo umoja wa mataifa unasema vinaendelea licha ya kutiwa saini kwa mkataba wa kuvisitisha juma moja lililopita.