Milioni 20 wakumbwa na njaa Sahel

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Chakuna ni haba eneo la Sahel

Umoja wa Mataifa unaomba zaidi ya dola bilioni 2 kuweza kuwapa watu milioni 20 chakula katika kanda ya Sahel barani Afrika.

Kanda hiyo inajumuisha nchi ya Sudan na Jamuhuri ya Afrika ya kati.

Taarifa kutoka katika ofisi ya mratibu wa misaada ya kibindamu ya Umoja huo barani Afrika, inasema migogoro katika nchi hizo na kwingineko Afrika imesababisha hali mbaya ya kibinadamu.

Wahisani waliweza tu kuchangisha asilimia sitini ya dola bilioni 1.7 ambazo Umoja wa Mataifa uliomba kuweza kushughuikia tatizo la njaa katika eneo la Sahel mwaka jana.

Mataifa yaliyo katika kanda hiyo iliyo Kusini mwa jangwa la Sahara, ambayo yanakumbwa na njaa ni pamoja na Mauritania, Gambia, Mali, Niger, Nigeria, Burkina Faso, Senegal na Cameroon.

Kwa mujibu wa Umoja huo, hali kwa jamii nyingi katika eneo hilo ni mbaya na inahitaji kushughulikiwa kwa dharura.

Hata hivyo kuna changamoto ya mataifa hisani kutoa mchango kwani baadhi yanakumbwa na msukosuko wa kiuchumi pamoja na kwamba tayari mataifa hayo yalichangisha pesa kwa ombi la awali la UN la dola bilioni 6.5.

Inaarifiwa watoto milioni tano walio chini ya umri wa miaka mitano, wanakumbwa na utapia mlo katika eneo la Sahel.

Kwa mujibu wa UN, watu milioni 2.5 ya wale wanaohitaji msaada wako katika hali mbaya sana na wanahitaji kushughulikiwa kwa dharura.