Wanawake taabani Afghanistan

Haki miliki ya picha AFP

Kundi la kupigania haki za kibinaadamu la human Rights watch limemtaka Rais wa Afghanistan Hamid Karzai kutotia saini mswada utakaopelekea kuwa vigumu kuwapata na hatia watu wanaotekeleza vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Mswada huo ulipitishwa na bunge la Afghanistan mwaka uliopita na unawazuia wachunguzi kuihoji familia ya mwaathiriwa.

Mwandishi wa BBC amesema kuwa sheria hiyo itapelekea kuwa vigumu kumshitaki mtu yeyote anayehusishwa na ukatili wa majumbani na ndoa za lazima kwa kuwa ni watu wa familia pekee wanaoweza kuwa mashahidi.

Makundi ya kupigania haki za kibinaadamu yamesema kuwa sheria hiyo ni pigo kwa haki za wanawake nchini Afghanistan.