Waandishi mashuhuri waishtumu Urusi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandishi wa Urusi

Zaidi ya waandishi 200 mashuhuri wa vitabu kutoka mataifa 30 wametia sahihi barua ya kuishtumu Urusi kwa kile wanachotaja kama vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza kufuatia kuidhinishwa kwa sheria za kukabiliana na wapenzi ya jinsia moja.

Katika taarifa ilioachapishwa kupitia gazeti la Guardian,waandishi hao wamesema kuwa hawawezi kunyamaza huku waandishi na wanahabari nchini Urusi wakilazimishwa kunyamaza la sivyo wakabiliwe na mashtaka kwa kutoa hisi zao.

Miongoni mwa waandishi hao ni washindi wa taji la Nobel Gunter Grass,Wole Soyinka,Elfriede Jelinek na Orhan Pamuk.Barua hiyo imechapishwa huku macho yote duniani yakielekezwa nchini Urusi, mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi mjini Socchi.

Barua hiyo ni miongoni mwa kampeni za shirika la kimataifa la waandishi PEN ambalo limekuwa likiangazia lile linalotaja kuwa kukabwa kwa uhuru wa kujieleza nchini Urusi chini ya uongozi wa rais Putin.