Polisi wa Kenya wakana kuteka ONLF

Image caption Vugu vugu la ONLF

Maafisa wawili wa Polisi nchini Kenya waliofikishwa mahakamani kwa kosa la kuwateka nyara maafisa wawili wakuu wa vuguvugu la (Ogaden National Liberation Front) la Ethiopia, wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni mbili kila mmoja au dola elfu ishirini na tatu.

Inaarifiwa maafisa hao waliwateka nyara Bwana Ali Ahmed Hussein na Sulub Abdi Ahmed mjini Nairobi na kuwapeleka nchini Ethiopia bila ya idhini yao.

Walikamatwa Januari 31. Wameachiliwa kwa dhamana baada ya kukana mashitaka.

Kundi la waasi la Ogaden National Liberation Front, ambalo linapigania kujitenga kwa eneo la Ogaden Mashariki mwa Ethiopia liliundwa mwaka 1984.

Maafisa hao walitekwa nyara nje ya mkahawa mmoja mjini Nairobi wa Arabian Cuisine Januari tarehe 26.

Kulingana na mkuu wa shirika la ujasusi la CID Kenya, watekaji nyara walitumia magari matatu katika shughuli hiyo ya utekaji nyara.

Haijulikani yaliko magari mengine matatu ingawa inaaminika yalipelekwa nchini Ethiopia.

Baadhi ya maafisa wa ONLF wamedai kuwa maafisa wa usalama wa Kenya na Ethiopia walishirikiana katika utekaji nyara huo.