Miili 8 yapatikana mgodini A. Kusini

Image caption Mgodi wa Doornkop uko Magharibi mwa Johannesburg.

Maafisa wa shughuli ya uokoaji nchini Afrika Kusini wanasema kuwa wamepata miili 8 ndani ya mgodi walimokuwa wamekwama wachimba migodi hao baada ya moto kuzuka na kuangukiwa na mawe wakiwa ndani ya mgodi huo.

Kwa mujibu wa serikali, Mfanyakazi mmoja angali hajapatikana katika mgodi wa Doornkop, Magharibi mwa Johannesburg.

Awali wachimba migodi wanane walipatikana wakiwa hai katika chumba kimoja chini ya ardhi ambako walijificha ili kuepuka madhara yoyote.

Moto ulizuka katika mgodi huo mnamo Jumanne umbali wa mita 1,700 chini ya ardhi.

Kiini cha moto huo bado hakijajulikana.

"Hali ni ya kusikitisha sana," alisema waziri wa madini Susan Shabangu.

"Lazima tuhakikishe tunafanya kila tuwezalo kubaini chanzo cha ajali hii ili tuweze kuzuia matukio kama haya katika siku za usoni.''

Eric Gcilitshana,wa chama cha wafanyakazi wa migodini (NUM), alisema kuwa miili hiyo ilipatikana Jumatano jioni.

''Hii ni siku kubwa ya huzuni kwetu NUM. Tunatoa rambi rambi zetu kwa familia za waathiriwa,'' alinukuliwa akisema Eric Gcilitshana.

Maafisa wa migodini awali, walielezea kuwa waokozi walikuwa wanakabiliwa na hali ngumu sana kuweza kuwafikia waathiriwa migodini kwa sababu ya moshi uliokuwa unafuka pamoja na mawe kuanguka.

Ingawa kiini cha ajali hiyo bado hakijajulikana, chama cha NUM kimependekeza kuwa tetemeko ndogo la ardhi huenda ndilo lilisababisha moto.

Kampuni ya Harmony Gold, imethibitisha kuwa eneo hilo linakumbwa na tetemo la ardhi ingawa la kiwango cha chini sana.

Chama cha NUM, kimetoa wito uchunguzi ufanywe mara moja ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Duru zinaarifu kuwa tukio hilo ndilo mbaya zaidi kukumba migodi ya Afrika Kusini tangu polisi kuwaua wafanyakazi wa migodini mwezi Julai mwaka 2009.