FBI inayo miili ya magaidi wa Westgate

Image caption Mmoja wa magaidi walioshambulia Westgate

Mkuu wa majeshi ya Kenya ameabia vyombo vya habari kuwa shirika la Ujasusi la Marekani FBI lilikabidhiwa miili ya magaidi walioshambulia jengo la Westgate nchini Kenya mwaka jana.

Karangi, ameyasema hayoalipokuwa akikitoa maelezo katika mkutano ulioandaliwa nchini Kenya na baraza la vyombo vya habari kuhusu ambavyo shambulizi hilo lilishughulikiwa.

Alisema kuwa majeshi yake hatimaye yaliweza kuwaua magaidi hao, siku mbili baada ya kuvamia Westgate tarehe 21 mwezi Septemba 2013.

Magaidi hao walifyatua risasi kiholela na kuwaua takriban watu 67 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

Bwana Karangi aliongeza kwamba baada ya shambulizi kuanza Jumamosi magaidi waliuawa siku iliyofuata.

''Miili ya magaidi hao ilikabidhiwa majasusi wa FBI,'' alisema Karangi ingawa hakutoa maelezo zaidi.

Washambuliaji wote wanne walikuwa wenye asili ya kisomali ingawa mmoja kati yao alikuwa ameishi zaidi nchini Norway

Maafisa wa usalama wakati huo wakipambana na magaidi hao walikuwa wametoa taarifa kuwa Westgate ilivamiwa na ilivamiwa na magaidi 12 ingawa idadi yao baadaye ilisemekana kuwa magaidi wanne pekee

Wanamgambo wa Somalia Al- Shabaab walidai kutekeleza mashambulizi hayo wakisema kuwa ilikuwa onyo kwa serikali ya Kenya kukoma kujihusisha na vita nchini Somalia ambako wanasadia majeshi ya Muungano wa Afrika kupambana dhidi ya Al Shabaab.