Milipuko yatikisa mji wa Cairo, Misri

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ni chini ya wiki mbili tangu shambulizi kubwa kutokea mjini Cairo

Mabomu mawili madogo yamelipuka karibu na mji mkuu wa Misri, Cairo katika eneo lenye barabara ya kupitia juu lenye kizuizi cha maafisa wa polisi.

Msemaji wa polisi Jenerali Mahmoud Farouk amesema kuwa mlipuko huo ulilenga magari mawili ya polisi yaliokuwa yameegeshwa katika eneo la Giza ili kulinda msikiti mmoja na medani kabla ya maombi ya siku ya ijumaa.

Maafisa wa afya wanasema kuwa maafisa sita wa polisi walijeruhiwa.

Mwandishi wa BBC katika eneo hilo amesema kuwa kuna uharibifu wa kiwango kidogo uliotokea.

Kumekuwa na maandamano kila ijumaa tangia jeshi limuondoe mamlakani aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi mnamo mwezi julai.