ICC kuchunguza uhalifu wa kivita CAR

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waisilamu wamekuwa wakishambuliwa nchini CAR na sasa wameanza kutoroka

Mwendesha mkuu wa mashitaka katika Mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC, Fatou Bensouda, ameanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Fatou Bensouda amesema kuwa amepokea ripoti za ukatili kutendewa makundi kadhaa yanayohusika na vita nchini humo.

Maelfu ya waisilamu tayari wameanza kutorokea nchini Cameroon na Chad.

CAR, ambayo ni moja ya mataifa masikini sana barani Afrika, imekuwa ikikumbwa na vurugu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa baada ya waasi waisilamu kuingia mamlakani kimabavu.

Bensouda alisema kuwa uchunguzi wake unahusu mauaji ya mamia ya watu, visa vya ubakaji na utumwa wa kingono , uharibifu wa mali uporaji, mateso, kuhamisha watu kwa nguvu na kutumia watoto kama wapiganaji.

Aliongeza kuwa katika matukio mengi, waathiriwa wameonekana kulengwa kwa misingi ya dini.

Ghasia nchini CAR zinaonekana kuchukua mkondo wa ukatili huku kukiwa na taarifa za makundi ya watu kuwaua wengine hadharani .

Mnamo siku ya Ijumaa asubuhi, maelfu ya waisilamu waliripotiwa kutoroka wakiwa wameabiri malori mjini Bangui kutafuta usalama katika mataifa jirani. Walisaidiwa na wanajeshi wa kulinda amani wa Chad.

Mmoja wa watu hao aliyeanguka kutoka kwenye lori aliuawa na umati wa watu huku mwili wake ukikatwa katwa.

Kiongozi wa waasi, Michel Djotodia, aliyeingia mamlakani kimabavu, alijiuzulu mwezi jana kama sehemu ya mkakati wa kuleta amani nchini humo lakini ghasia zimeendelea tangu hapo.