Mazungumzo ya amani kuendelea Addis

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu waliokimbia makwao nchini Sudan Kusini

Mazungumzo ya amani kati ya Waasi na serikali ya Sudan Kusini yatarejelewa tena leo mjini Adis Ababa Ethiopia.

Pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mapema mwezi uliopita baada ya shinikizo kutoka jamii ya kimataifa.

Waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar, na serikali ya rais Salva Kirr wamekuwa wakisisitiza kwamba zinatii makubaliano hayo licha ya kwamba bado mapigano yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini.

Mapigano hayo yaliyodumu kwa zaidi ya miezi miwili, yamekuwa na athari kubwa katika taifa hilo changa zaidi duniani.

Watu wakabiliwa na baa la njaa

Image caption Watu waliokimbia makwao nchini Sudan Kusini wakila nje katika kambi moja ya muda

Ripoti zinasema kuwa maelfu ya watu wameuawana zaidi ya watu laki saba wamekimbia makwao.

Jumuiya ya Maendeleo ya kanda ya Afrika Mashariki na Kati IGAD, tayari imetuma ujumbe nchini Sudan Kusini kuchunguza utekelezwaji wa mkataba huo wa amani.

Lakini wanajeshi wa serikali ya Salva Kirr na wanajeshi watiifu kwa makamu wa rais wa zamani wamekuwa wakiendeleza mapigano huku wakishutumiana hadharani, kabla ya awamu ya pili ya mazungumzo hayo.

Mapigano hayo nchini Sudan Kusini yalianza Desemba mwaka uliopita, kama mapigano kati ya makundi hasimu jeshini.

Umoja wa mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni tatu nukta saba wanahitaji misaada ya dharura nchini humo, ikiwa ni pamoja na chukula maji na dawa kufuati mzozo huo..